1.moyo umefunga penzi, la mahabubu fulani
keshapo ninalienzi, lisidondoke changani
wanijiliapo wezi, huwa mfarakanoni
ajabu moja ni kuwa, simjui mja huyo
2.hapata wivu wa nafsi, nikaungua rohoni
nikabanguliwa rasi, ugonjwa nisibaini
tabu zisizo kiasi, kuninahili moyoni
ajabu moja ni kuwa, simjui mja huyo
3.mapenzi haya ya ghibu, kuwa kwake siamini
yalianza taratibu, kuingia akilini
sasa ndo nahisi tabu, mapenzi kunitahini
ajabu moja ni kuwa, simjui mja huyo
4.awali lihisi tamu, na furahiko ndotoni
hatekenya milizamu, nilalapo kitandani
kumbe najinywesha sumu, ya teseko maishani
ajabu moja ni kuwa, simjui mja huyo
5.akija huchekacheka, na kudekewa mwilini
pwani tukarukaruka, mfano mahayawani
sabahi kikurupuka, pekee hajibaini
ajabu moja ni kuwa, simjui mja huyo
6.ana uso wa duara, huburudisha aini
na kifua cha kufura, mwenyezi hakumhini
miguu ilo imara, hufurahisha machoni
ajabu moja ni kuwa, simjui mja huyo
7.ana macho ya kung'ara, mithali yake sioni
kope zake zimechora, mfano wa asumini
na libasi za sitara, kama zatoka peponi
ajabu moja ni kuwa, simjui mja huyo
8.nimekwenda kwa waganga, zindiko kulibaini
mitishamba kunisinga, kama mwari mafundoni
hirizi wakanifunga, kuenea maungoni
ajabu moja ni kuwa, simjui mja huyo
9.kila jambo halikuwa, ndugu nisaidieni
vitabu nimebukuwa, vya uchawi na vya dini
nimebaki naungua, mola hanipi idhini
ajabu moja ni kuwa, simjui mja huyo
10.wakatabahu shairi, wajuvi nielezeni
kwa wale wanofasiri, ruwiya za mapenzini
naomba yenu nadhari, asaa nimbaini
ajabu moja ni kuwa, simjui mja huyo
Thursday 24 January 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment