Wednesday 23 January 2008

LADHA YA USHAIRI

AKILI KUZIHARIBU

1.wapungufu wa akili, kisha tunaziharibu
kwa maji yalo dhalili, twaadhirika ajabu
wasomi wenye adili, vileo huwatulubu
pombe hutudhalulusha, na kurufaisha akili

2.kwa zetu mbaya fiili, mola anatuadhibu
makatazo hatujali, tu wima kama bawabu
mwisho wa siku twafeli, peponi twajitanibu
pombe hutudhalilisha, na kurufaisha akili

3.twazitia uasili, amali ziso adabu
vinywaji vyenye mushkeli, twaviita vya mababu
mawazo ya kibaghili, viumbe yametusibu
pombe hutudhalilisha, na kurufaisha akili

4.wa moja hashiki mbili, ya busara na ulabu
ubongo hatuujali, hulegeza sukurubu
nyoyo hupata ajali, tukawa kama mabubu
pombe hutudhalilisha, na kurufaisha akili

5.himila wanohimili, bure hujitia tabu
hufura yao miili, na nyuso kufanya gubu
mtoto akiwasili, wakunga huwatulubu
pombe hutudhalilisha, na kurufaisha akili

6.nawaasa kula hali, mtenzi nawaadibu
kwa uchache wa kauli, penye makosa natubu
natetea maadili, siandiki kwa ghadhabu
pombe hutudhalilisha, na kurufaisha akili

MAISHA
1.maisha yanatutesa, na kutunyima huruma
hupatwa na vingi visa, kwa chukizo na hujuma
wengi hupata garasa, hata wanapojituma

2.maisha yana mikasa, kila siku kila juma
dunia hutikisika, kwa dhambi zenye kuuma
kama tulo na darasa, matusi tunavyosema

3.maisha yana makosa, mwanadamu hana jema
kama tulo na ruhusa, kwa vitendo vya uchama
tena hayo yote tisa, kumi kumtusi mama?

4.maisha yana usasa, cha zamani siyo chema
mcha mungu hukutesa, kwa kuwarudisha nyuma
ukihudhuria kesa, na fedha hukuazima

5.maisha yana anasa, akili usipotuma
vitamu hutovikosa, madhambi ukiyachuma
mwisho wale vibubusa, hulia na kuchutama

UTUMWA WA MAOVU
1.utumwaji wa maovu, hudhihaki milizamu
hukomaa kama kovu, ridhio lake ni hamu
moyo hupata machovu, na kulia madhulumu
ila mtumwa wa dhambi, hutubia akaacha

2.ovu halina utuvu, hufanya mwenye nidhamu
keshapo hushika shavu, kulia kibahaimu
akidai maonevu, yeye yamemstakimu
ila ajabu ya mungu, kesho hurudia tena!

3.hana ustahamilivu, muovu akikasimu
humnasa kama wavu, ubaya kwa wanadamu
tena huwa ni shupavu, hata jambole litimu
hapo hupata wasaa, akamkumbuka mungu

4.watovu wa usikivu, wovu washikwapo hamu
hupatwa na maumivu, katika zao fahamu
hawawi ni wakatavu, hudhani ni isilamu
hawaombeleki dua, nyoyo zimepigwa chapa

5.na hivi vina vya VU, vinaninyima kalamu
mfano wake VVU, umuri kunidhulumu
hapa nafanya kitovu, nimezidiwa elimu
vina vimeniishia, shairi laendelea.

No comments: